Saturday, March 17, 2012

Madhara ya kuwa na marafiki waliokata tamaa

Mara nyingi nimeeleza katika mafundisho yangu kwamba mawazo yetu yakitupa majibu kwamba vitu tunavyotaka kuvifanya vinawezekana bila shaka tunaweza kutenda hata kama vitakuwa vigumu kiasi gani kwa sababu mawazo yanayotuongoza hupita vikwazo vya matatizo yetu.

Kwa upande mwingine chochote tunachoamini kuwa hakiwezekani, hatuwezi kuwa na msukumo wa kujaribu kwa vile hofu ya kushindwa huongeza udhaifu wa mwili, wanasaikolojia maarufu akiwemo Lakshmi Aiyer wamethibitisha hili.

Tafiti za kitaalamu zinaonesha kuwa, tabia za watu hujengwa na ndugu, marafiki au mazingira yanayowazunguka kila siku. Hii ina maana kwamba kama tutakuwa na marafiki au ndugu waliokata tamaa ya maisha upo uwezekano mkubwa wa kuathirika kisaikolojia.

Imebainika kwamba hata wanaume na wanawake wanaojiingiza kwenye uhusiano wa mapenzi wengi wao ni wale ‘walioathirika’ na kukutana kwao kila siku kwenye mazingira wanayoishi.

Bila shaka wewe msomaji wangu unaweza kufanya utafiti wako na kugundua kuwa asilimia 80-90 ya wanandoa uhusiano wao ulianza wakati wakiwa pamoja shuleni, kazini au mtaani. Ukweli huu unaweza kuwa msingi wa somo hili juu ya athari za marafiki kwenye maisha yetu.

Ikumbukwe kuwa maisha ni mipango, lakini si kila kitu tunachopanga kinakuwa kimetokana na juhudi zetu za kufikiri. Wajuzi wa elimu ya maisha wanasema, asilimia kubwa ya mipango na tabia ya mwanadamu ni ya kuambukizwa kutoka upande wa pili unaomzunguka.

Wengi wetu tunaambukizwa kutumia vinywaji fulani si kwa sababu tulipanga kuvitumia, lakini mawazo yetu yalitekwa na matangazo kwenye luninga na redio yaliyokuwa yanatushawishi bila sisi wenyewe kujua na tukajikuta siku moja tunaamua kunywa.

Hii ina maana kwamba, mtu mmoja tu mwenye mawazo ya kushindwa, aliyekata tamaa anatosha kabisa kutuondolea shauku ya kufanikiwa, endapo atapata nafasi ya kutueleza kila mawazo yake ya kukata tamaa.

Naamini ndoa nyingi zinavunjika siku hizi kwa sababu, baadhi ya wanawake/wanaume wanatoa nafasi kwa rafiki zao kuwapandikizia udhaifu. “Mumeo hafai ni mhuni sana, anakutesa. Mkeo mbaya hamuendani naye mkitembea hampendezi.”

Kwenye maisha haya tunaishi na marafiki hatari wanaotuambia kuwa hatuwezi kufanikiwa kwa sababu hatujasoma, hatuna mitaji ya biashara au serikali haijaweka fursa za vijana kuendelea. Watu wa aina hii tuko nao kila siku kazini na huko kwenye makazi yetu, wanatulisha hali ya kukata tamaa bila sisi wenyewe kujitambua.

Wengine wanatuvunja moyo wa kufanya kazi kwa bidii kwa kutuambia: “Kwenye kampuni yetu tunafanya kazi sana, halafu mshahara mdogo.” Kwa kuwa tumewapa nafasi ya kutuambia na sisi tunawasikiliza taratibu tunajikuta tunachukia kazi na kuona ni bora kuacha.

Naamini vijana wezangu mmeacha kufanya vitu vingi kwenye maisha yenu kwa sababu rafiki zenu waliwavunja moyo. Tumeacha wapenzi wetu kwa ushawishi wa wengine, tumeuza viwanja, tumejiingiza kwenye tabia mbaya, tumekata tamaa kimaisha kwa sababu ya ndugu zetu.

Kwa msingi huu, natoa ushauri kuwa kila mtu anatakiwa kuwa makini na rafiki aliyekata tamaa. Tusikubali kuruhusu mawazo yao yaongoze maisha yetu. Ulimwengu wa leo unahitaji marafiki wenye kutia moyo, watakaotuhamasisha kujenga nyumba, tununue viwanja, kubana matumizi na kuachana kabisa na tabia mbaya.

Lazima tuhakikishe kuwa mawazo yetu yanakuwa na nafasi kubwa kwa wenzetu siyo kusikiliza maneno ya kuvunja moyo kila siku. Kujihami kwetu na madhara ya kuvunjwa moyo ni kupingana na mtazamo wa kushindwa unapoletwa kwetu na rafiki zetu.

Baada ya kusoma mada hii hebu kuwa mtu wa kwanza kujitambua, hakikisha kuwa akili yako haiingizi mawazo ya kushindwa maisha, haufikirii kufa, haukati tamaa kwenye jitihada zako za kutafuta maisha na siku zote lazima tuseme.
HAKUNA LISILOWEZEKANA.

Related Posts by Categories



No comments:

Post a Comment