Saturday, March 17, 2012

Migogoro ya watoto wa kambo na ufumbuzi wake

Kwa mujibu wa Becnel, mwandishi mashuhuri nchini Marekani anaeleza kwamba, familia ambazo zinaongoza kwa migogoro ni zile ambazo zimeundwa na wazazi ambao wana watoto wa nje ya ndoa au kwa lugha ya hapa nyumbani ‘watoto wa kambo’.

Katika hali ya kawaida imebainika kuwa ni vigumu kuwalea pamoja watoto wazawa na wale wa kufikia. Wanawake wengi wanalalamika kuteswa kwenye ndoa zao na wengine kuamua kuachika kwa kukimbia matatizo ya watoto hawa.

Pamoja na hayo, watoto wa kambo nao kwa upande wao wamekuwa wakitia kasoro malezi wanayopewa na walezi wao, bila kujali ni baba au mama wa kufikia. Uchunguzi unaonesha kuwa ni familia chache zinazoishi kwa amani kwa kuwa na watoto wa baba au mama tofauti.

Inatajwa kuwa vigumu kwa mama kugawa upendo sawa kwa wanae na wale wa mumewe, kadhalika baba hajitumi sana kuwapenda watoto aliozaa mkewe kwa mwanaume mwingine, ingawa kwa kiwango fulani wanaume wanatajwa kuweza zaidi ya wanawake.

Kimsingi tatizo la familia mseto ni kubwa ambalo halijapatiwa ufumbuzi wa kimawazo na wanandoa wengi. Watu wengi husukumwa na mvuto wa kimapenzi na kuamua kuoana haraka bila kupima na kuthibitisha uwezo wao wa kuishi na watoto wa kambo.

Ni rahisi mwanaume au mwanamke kusema: “usijali mpenzi tutaoana na watoto wako nitawalea bila matatizo” Hii ni kauli tu, lakini ukweli ni mgumu kuufuata, kwani nia ya kupenda lazima iwe na pande mbili yaani watoto na walezi.

Kuna wanawake ambao hujitahidi kuonesha upendo kwa watoto wa kufikia, lakini hukumbana na vikwazo vya wao kutopendwa na watoto hao. Huu ndiyo ukweli, kwamba unaweza kuwapenda wasikupende au wakakupenda lakini wewe usiwapende.

Natumaini hapo ulipo msomaji wangu utaendelea kufanya uchunguzi wako na hakika utabaini matatizo mengi yakiwemo pia ya urithi wa mali. Lakini wakati ukifanya hivyo ni vyema tukajifunza ufumbuzi wa matatizo ya watoto wa kambo kwa kuangalia yafuatayo:

KWANZA: Wazazi hawafundishi na kuweka usawa wa malezi na haki za watoto bila kujali kama wamewazaa au ni wa kufikia. Ni vyema walezi wakajenga tabia ya kugawa haki za kimaisha kwa watoto kwa usawa. Hii itawaondolea chuki watoto hasa wale wa kufikia ambao huhisi kutopedwa.

PILI: Watoto wa kambo huwa si wepesi kutii amri za walezi wao. Hivyo ni jukumu la baba au mama wa mtoto husika kuwa na msimamo mkali na kuhakikisha anamlazimisha mtoto wake kumtii mlezi wake, hii ikiambatana na kutomuunga mkono kwa urahisi pale anapolalamika kutopendwa au kutendewa sivyo.

TATU: Watoto wazawa hujihesabia haki na kuwadharau wenzao. Ni jukumu la wanandoa kuhubiri haki za watoto wote na kuondoa mtazamo miongoni mwa watoto kwa kuwagawa hawa wangu na wale wa mwingine na hivyo kuweka upendeleo wa kimalezi.

NNE: Watoto wa kufikia huwa na tabia zile walizokuzwa nazo, hivyo inawezekana zisiwapendeze walezi. Hilo ni jukumu la walezi kuwavumilia na kuwabadilisha taratibu. Kwa kushirikiana kati ya mzazi na mlezi. Ni jambo baya kugawanyika katika msimamo na mafunzo ya mtoto wa kambo kwani kwa kufanya hivyo kutamfanya mtoto amsikilize zaidi mzazi kuliko mlezi.

TANO: Saikolojia inatambua kuwepo kwa fikra potofu baina ya walezi na watoto wa kambo, mara nyingi upande mmoja unapotenda jambo baya, upande uliotendewa huamini kuwa watendaji wamefanya hivyo kwa sababu ya ukambo wakati kumbe makosa yaliyotokea ni ya kibinadamu tu.

Hivyo,ni jukumu la watoto na walezi kupokea makosa hayo kama ya kibinadamu na kuacha kukimbilia kuyatengenezea taswira ya ukambo na kujikuta wakizalisha hasira nyingi na chuki ambazo wasingezifikia kama wangewachukulia hao kama watoto na walezi wao tu.

Mwisho ni wajibu wa walezi kushirikiana kuwalea watoto wa kufikia huku msukumo mkubwa ukitoka upande wa mzazi ambaye atahakikisha kwa makusudi anawajengea wanae tabia ya kumheshimu mlezi wao kuliko hata yeye. Hii itamtia nguvu mlezi na kujiona kama naye ni mzazi halisi na hivyo kuondoa utengano na migogoro ambayo familia nyingi zimejikuta zikigawanyika kutokana na watoto wa kambo.

Related Posts by Categories



No comments:

Post a Comment