Watu wamekuwa wakifanyiana ukatili, nchi zinapigana vita kwa sababu ambazo kama mwanzo zingepata wajuzi wa kuitatua isingeleta madhara makubwa (L. Ron Hubbard, Mtafiti wa Sayansi ya Jamii kutoka Marekani anathibitisha hili pia). Zifuatazo ni mbinu za kufikia makubaliano na mtu uliyekosana naye kwa sababu za kimaisha.
KWANZA : Mgogoro unapotokea baina ya mtu na mtu au taifa na taifa, kitu cha kwanza kabisa kufanyika ni kwa wahusika kutambua kuwa wameingia katika mgogoro na hivyo kutazama kwa kina madhara ya mgogoro na kuamua kutuliza jazba zao kwa lengo la kuangalia namna ya kumaliza tatizo kwa amani.
Hapa anayesuluhisha hatakiwi kutafuta nani mwenye makosa katika mgogoro huo bali ni wakati wa kutatua tatizo, huku hilo la nani kakosa likishughulikiwa baadaye.
PILI : Kwenye mgogoro kila mtu hupenda kusikilizwa akiamini kuwa ana sababu za msingi zilizomfanya akasirike au akorofishane na mwenzake. Hivyo ni wajibu kwa watu wenye elimu ya kutatua migogoro kuwapa nafasi wahusika wa pande zote mbili waseme yaliyo mioyoni mwao, hata kama yatakuwa yamesheheni matusi na uongo.
Usimkatize mwenzako anapotoa maelezo yake, nyamaza umsikilize mpaka mwisho akimaliza na wewe eleza yako kwa upole, kama una haki jamii itakupa.
TATU : Usikimbilie kujihukumu hasa pale wasuluhishi wanapojaribu kuchambua mambo kwa kuonesha dalili za kukuzonga na pengine kukuhukumu. “Ok, kama mimi nina makosa basi niacheni kaeni ninyi wasafi,” usiseme hivyo vumilia lawama na pointi yako ya msingi iwe ni kwenye busara ya kulimaza tatizo ukiwa unafahamu fika kuwa kuishi na familia, mke/mume kwa mgogoro si jambo zuri.
NNE : Unapokuwa katika safari ya kutaka suluhu pendelea sana kuunga mkono yale yanayozungumzwa kwenye kikao au anayozungumza mwenzako. “Ni kweli, ni kweli kabisa, hapo umesema sawa, nakubaliana na wewe”. Kauli za kukubali kama hizi zina nguvu kubwa ya kuwafanya wajumbe au mgomvi mwenzako anyonywe hasira na kukuona ni mtu mwelewa unayestahili kusamehewa na kupewa nafasi ya kujisahihisha.
TANO : Kama utaona mgomvi wako bado amejaa hasira kiasi cha kutotaka kukusikiliza, sitisha mapatano na umruhusu aondoke au wewe uachane naye kwa muda. “Naona bado una hasira nyingi, tulia hasira zikipungua tutazungumza”.
Unapompa mwenzako muda wa zaidi wa kutafakari, kiwango cha hasira hushuka na pengine kufikiria zaidi madhara ya kugombana. Usilazimishe kuwasuluhisha watu wakati unaona wako kwenye muwako wa hasira, ukifanya hivyo utakuza tatizo.
SITA : Mtakapofikia katika hatua ya maelewano na ukabaini kuwa wewe ulikuwa na makosa katika mgogoro huo, uungwana unakutaka uwe mwepesi kukiri kosa na kutaka kumaliza tatizo. “Niliteleza naomba unisamehe.” Lakini hata kama umeona mwenzako ana makosa ila hataki kukubaliana na wewe, kuwa tayari kubeba lawama kwa lengo la kumaliza tatizo, kwani gharama ya kubeba kosa ni ndogo ukilinganisha na ile ya kuendeleza mgogoro.
SABA : Jambo kubwa la mwisho linaloweza kusaidia kutatua migogoro ni kutumia nguvu ya ufahamu wako wa mambo.
Kama unaishi na mkeo nyumba moja kwa miaka mingi, unatakiwa kumfahamu tabia zake na kuzichukulia hadhari, vivyo hivyo bosi wako, wafanyakazi wenzako, wanafunzi wenzio na waalimu wako, lazima uwafahamu tabia zao. Hii itakusaidia kutoingia katika migogoro nao kwa vile utakuwa unafahamu mambo wasiyoyapenda.
Saturday, March 17, 2012
HATUA SABA ZA KUTATUA MIGOGORO INAYOTUKABILI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment