Baada ya kuanza kujiuliza na kuyatambua malengo yako huku ukiandika kila wazo linalokujia akilini, fuata hatua zifuatazo:
1. JENGA PICHA AKILINI MWAKO
Jenga  taswira ya kitu unachokitaka akilini mwako. Picha unayoijenga lazima  iwe kubwa. Fikiria jinsi utakavyokuwa na mafanikio makubwa maishani  katika kile ulichochagua kukifanya. Jione tayari ukiwa katika mafanikio  ambayo ulikuwa ukiyatamani kwa siku nyingi.
 Jitazame furaha  utakayokuwa nayo na jinsi utakavyoyamudu maisha ya mafanikio. Panga  malengo ya muda mrefu. Usifikirie kuwa ulichokiwaza kitatokea kesho,  jipe muda hata wa miaka kumi au zaidi, usiogope kufikiria mambo makubwa  yanayohitaji muda mrefu kukamilika. Kuanzia hapo, endelea na hatua ya  pili.
2. YARAHISISHE MALENGO YAKO
Yawezekana malengo yako ni  makubwa sana kiasi cha kukuzidi. Hiyo isikutishe, yarahisishe malengo  yako. Kivipi? Kama malengo yako ni kuwa na mafanikio makubwa maishani  baada ya miaka kumi, ugawanye muda wako katika sehemu ndogondogo.
Kwa  mfano unaweza kuanza kugawanya miaka kumi kwa mbili, yaani baada ya  miaka mitano uwe angalau umefikia nusu ya kile ulichokiwaza awali. Baada  ya hapo igawanye miaka mitano kupata mwaka mmoja mmoja.
Jiulize  kwa kila mwaka utafanya nini ili kuyakaribia mafanikio. Weka ratiba na  mipango yako kwa maandishi. Ugawanye mwaka kupata miezi, jiulize  utafanya nini mwezi wa kwanza, wa pili hadi mwaka uishe. Hakikisha  unaandika kila kinachokujia akilini.
Endelea kurahisisha malengo  yako kwa kujiuliza ndani ya miezi sita utakuwa tayari umefanya nini,  shuka mpaka miezi mitatu kisha malizia kwa kila mwezi mmoja. Utaona  kwamba lengo unalotarajia kulifanikisha kwa kipindi cha miaka kumi  umelirahisisha mpaka kwenye mwezi mmoja.
 Usiishie hapo, mwezi  ugawanye kwenye wiki, kisha malizia kwenye siku. Jiulize kila siku  utafanya nini ili kuelekea kwenye lengo lako kubwa unalotaka litimie  baada ya miaka kumi. Hapo utaanza kuona umuhimu wa kutumia muda wako  vizuri, hakuna muda wa kupoteza.
3. ANZA UTEKELEZAJI
Anza  utekelezaji wa malengo yako mara moja.  Hakikisha kila saa inayopita  umefanya jambo ili kupalilia malengo yako. Hakikisha unafuata ratiba  uliyojipangia, usisubiri mtu mwingine aje kukukumbusha kuhusu malengo  uliyoyapanga. Tembea na karatasi au kitabu ulichoandika malengo yako na  endelea kujikumbusha kila siku juu ya kile unachotaka kitokee.
Mwanasaikolojia  mmoja mashuhuri aliwahi kuandika kuwa: Mafanikio siyo tukio unaloweza  kulisubiri litokee bali ni hatua unayochukua kuyafikia. Ukianza  kufikiria mafanikio, tayari umeanza kufanikiwa, ukiweza kupanga malengo  na kuanza kuyafanyia kazi, tayari umo ndani ya mafanikio.
Usisubiri  itokee siku ambayo utalala halafu ukiamka asubuhi ukute yale uliyokuwa  unayataka yametokea. Malengo yako lazima yakutese usiku na mchana. Watu  wote waliofanikiwa hawakufika hapo kwa bahati, walipanga malengo na  wakayafanyia kazi.
MAMBO YA KUZINGATIA KUELEKEA MAFANIKIO
Kwa  kuwa maisha ni kama safari na malengo ndiyo dira, ukianza kuyafanyia  kazi malengo yako utagundua unatakiwa kufanya nini ili safari yako ya  maisha iwe rahisi. Lazima ufahamu mambo muhimu yatakayokusaidia  kurahisisha safari yako kuelekea mafanikio.
Saturday, March 17, 2012
Namna ya kupanga malengo maishani II
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment