Siku zote hatutaacha  kuzungumza juu ya mapenzi kwani ni ukweli usiopingika kwamba mapenzi  yanachukua nafasi kubwa sana katika maisha yetu.
Tunafanya kazi  usiku na mchana, tunahangaika huku na huko, lakini mwisho tunafikiria  jinsi gani tutaboresha na kufurahia maisha na wapenzi wetu.
Mpenzi  msomaji wangu, katika maisha ya kimapenzi uaminifu ni kitu cha msingi.  Bila uaminifu baina ya wawili waliotokea kupendana, hakuna mapenzi na  hata safari yao inaweza isifike mbali.
Kwa sababu hiyo ndiyo maana  wataalam wa mapenzi mara kwa mara wamekuwa wakizungumzia suala hili kwa  nguvu zote wakiamini ni mhimili muhimu sana katika mapenzi.
Ifahamike  kwamba uaminifu unaweza kujengwa. Kwa mfano unaweza kuingia kwenye  uhusiano na mtu kisha ukapata malalamiko kutoka kwake kuwa, wewe si  muaminifu. Katika mazingira haya ni suala la kujiangalia tu na ili  kuepusha mgogoro, tengeneza mazingira ya kumfanya huyo mpenzi wako  akuamini.
Unafanyaje? Zifuatazo ni baadhi ya mbinu zinazoweza kukusaidia katika kujenga uaminifu katika ndoa yako:
1. Kuwa mkweli
Hakuna  kitu kibaya kama kuwa muongo kwa mwenzi wako. Unamfanya aamini kwamba  wewe si muaminifu kwake na ndiyo maana unadanganya bila sababu za  msingi. Kwa maana hiyo unachotakiwa kufanya ni kuwa mkweli kwake katika  kila jambo.
2. Timiza kwa wakati
Uaminifu pia unajengwa kwa  kutimiza mambo kadha wa kadha kwa mwenza wako hasa pale unapotoa ahadi.  Kwa mfano mmekubaliana mkutane maeneo flani saa 2:00 asubuhi, hakikisha  unakuwa pale kwa wakati. Huo ni mfano tu lakini kuna mambo mengi ambayo  unatakiwa kumtimiza mtu wako kwa wakati ili kujenga mazingira ya wewe  kuaminika.
3. Weka mipaka
Kama wewe ni mwanaume hakikisha  unajiwekea mipaka ya mazoea na wasichana wengine. Punguza mazoea yasiyo  ya lazima nao kwani hiyo inaweza kumjengea mpenzi wako hisia kwamba  unamsaliti.
Epuka kuwapa namba za simu watu ambao wanaweza kukuletea  usumbufu kwa mkeo. Epuka utani wa kijinga na watu wa jinsia nyingine.  Hii ni kwa mwanaume na mwanamke.
Ukijiwekea mipaka madhubuti utakuwa unamuweka mwenza wako katika mazingira ya kukuamini kwamba huwezi kushawishika kumsaliti.
4. Jiamini mwenyewe
Hili  ni la msingi sana. Kama unataka kujenga mazingira ya kuaminiwa anza  kujiamini mwenyewe. Kama utashindwa kujiamini hata mpenzi wako hawezi  kukuamini na matokeo uaminifu kati yenu hauwezi kuchukua nafasi.
5. Weka mambo sawa
Kwa  mfano mkeo anakutuhumu kuwa na uhusiano na mwanamke mwingine. Kumbuka  hisia hizo hata kama hazina ukweli usipojitahidi kuziondoa kwake, atajua  ni kweli unamsaliti na ataamini hivyo katika kila siku ya maisha yake.
Kwa  mazingira hayo elewa uaminifu hauwezi kuwepo kati yenu hivyo  unachotakiwa kufanya ni kuhakikisha unamuweka sawa mpenzi wako na  kumfanya aondoe hisia hizo. Kwa kufanya hivyo utakuwa umejenga mazingira  ya uaminifu kati yenu.
Saturday, March 17, 2012
Namna unavyoweza kujenga uaminifu katika ndoa yako
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment