Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha British Columbia (UBC), wanasaidia majibu ya swali hili kulingana na uchunguzi walioufanya na kuuchapisha katika Jarida la ‘Journal Science’ la Machi 21, 2008 kwamba watu wengi hutumia fedha zao kununua furaha.
Inaelezwa katika ripoti zao kwamba watu wengi wanapokuwa na fedha hupenda kuzitumia kwa kununua kadi, zawadi kwa wawapendao, kukusanyika pamoja na marafiki ili kushiriki furaha za pamoja kwa kunywa, kula na kustarehe sehemu mbalimbali.
“Ni ukweli ulio wazi kwamba fedha nyingi hutumika kununua furaha. Tumeona hili katika uchunguzi wetu uliohusisha zaidi ya watu 630 kutoka nchini Marekani ambapo asilimia 87 kati ya tuliowadodosa kuhusu matumizi ya fedha zao walisema wanazitumia kununulia mahitaji na vitu vidogovidodo zikiwemo zawadi na nguo, ” anasema Profesa Elizabeth Dunn mmoja wa watafiti wa UBC.
Utafiti huo wa kitaalamu una maana kubwa katika maisha ya binadamu hasa linapokuja suala la mafanikio. Ukiangalia kwa makini, watu wengi hutumia fedha kuleta furaha katika maisha yao, jambo ambalo ni hatari kimaendeleo.
Uhusiano wa matumizi ya fedha, tabia za mwanadamu na kanuni za mafanikio ni mambo yanayohitaji elimu ili kumfanya mtu atambue hasara za ununuzi wa furaha ambazo anazipata pale anapotoa fedha zake kujipatia vitu anavyovipenda.
Ni mambo yaliyo wazi kwamba, mtu anaponunua pombe au kuandaa pati ya kuzaliwa kwake, hufurahi, lakini kanuni za maendeleo haziko kwenye msingi wa furaha ya kununua kwa siku moja bali matarajio ya furaha.
Katika hali ya kawaida, wengi hawataki kutarajia furaha bali kufurahi kila wanapohitaji. Ili kujua zaidi kuhusu hali hii, ni vema tukajiuliza ni nani aliyepata kujenga nyumba huku akifurahi? Tunasikia kila siku watu wakisema, “Jamaa amekuwa bahili sana, sijui anajenga nyumba?” au “Maisha yangu yamekuwa magumu sana siku hizi namalizia kibanda changu.”
Tafsiri ya kumalizia kibanda ni maisha magumu na ubahili, lakini baada ya nyumba kukamilika kile kinachotajwa kama furaha ya mafanikio hujitokeza na kumfanya mhusika kujua kuwa kipindi cha ubahili kilikuwa ni cha furaha pia, tofauti na mtazamo wa wengi.
Watu huniuliza; kwa nini fedha zangu hazikai, yaani kila nikizipata zinakwisha hivihivi wala sijui hata nimezifanyia nini? Waulizao maswali ya namna hii huwa hawajui kuwa maisha yao wameyaelekeza katika kununua furaha.
Wengi wetu tumekuwa wepesi kutii tamaa kwa kununua mavazi, kwenda saluni, kula vyakula vinono, kufanya starehe na kusahau kufanya mambo ya msingi ya kujijengea uwezo wa kutufikisha kwenye furaha ya muda mrefu yaani kuishi maisha yenye mafanikio makubwa.
Bila shaka kila anayetaka kufanikiwa lazima aache kuwa mteja wa furaha, azuie fedha zake zisitoke kwa lengo la kuufurahisha mwili, kujenga urafiki na watu wengine na kujikweza.
Mtu yeyote akitaka kujua kama anaishi kwa kununua furaha achukue kalamu na karatasi, aorodheshe matumizi yake kwa mwezi atagundua asilimia zaidi ya 85 ya mshahara wake, kama walivyosema watafiti wa UBC, zimetumika kununulia furaha.
Katika orodha hiyo atakuta amewapa ofa watu fulani, alimhonga msichana, alilipia kiingilio cha muziki, alilipa pango kwenye nyumba ya kulala wageni, alinunua pombe, yote hayo ni mambo ya fedha kununua furaha.
Nimalize kwa kusema kwamba, makala haya yanashauri kila mtu awe tayari kuishi kwa kutegemea furaha si kununua furaha kwa sababu ni hasara kufanya hivyo.
Bila shaka wanaotegemea furaha wataweka benki fedha zao ili waanzishie miradi, watanunua mifuko ya simenti, watasomesha watoto wao, watanunua viwanja na kadhalika, mambo ambayo ukiyatazama kwa juujuu utadhani yanapunguza uwezo fulani kwenye maisha lakini kumbe ndiyo mafanikio yenyewe.
Saturday, March 17, 2012
Je Ni Kweli Fedha Hununua Furaha
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment