Familia nyingi na hasa watoto wamekuwa wakikatazwa na wazazi wao kuangalia sinema kwa fikra kwamba zinapumbaza na kupoteza muda, jambo ambalo wanasaikolojia wanapingana nalo.
Mwanasaikolojia Dorothy Halla-Poe kutoka Marekani anabainisha kitu tofauti na mtazamo wa wengi kuwa, kazi ya filamu si burudani pekee, bali tafiti zinaonyesha kuwa ni njia yenye mafanikio makubwa katika kujifunza mambo na kutibu baadhi ya matatizo yanayowakabili wanadamu.
Eti, tuamini kwamba sinema zinafundisha na kutatua shida zetu? Jibu ni ndiyo kwa asilimia mia moja, kwani ndani ya filamu uanadamu wetu unakamilishwa kwa kujifunza kupitia kusikia, kuhisi na kutafakari, mambo ambayo yanapatikana ndani ya filamu.
Hakuna ubishi kwamba uchaguzi wa simulizi, visa na tungo zinazopatikana kwenye filamu ndiyo jambo pekee linalohitajika kuzingatiwa, hii ikiwa na maana kwamba kujifunza, kujitibu matatizo yetu kunaanzia kwenye kile tunachotaka kukitazama ndani ya filamu.
Upo ushahidi wa kutosha juu ya watu wenye matatizo ya hisia za kimapenzi kumaliza ugonjwa wao kwa kutazama sinema za ngono huku wengine wakitajwa kujengwa kiimani, ujasiri na uvumilivu kupitia michezo ya kuigiza.
Kwa msingi huo hatuwezi kupuuza utazamaji wa sinema kwani inawezekana kuihamasisha jamii yetu kuwa hodari katika mambo wanayoyaona yakitendwa na waigizaji.
Kupitia filamu tunaweza kuwapatia watoto wetu moyo wa kishujaa mithili ya michezo inayoigizwa na wasanii. “Mimi Rambo” “Basi mimi Schwarzenegger” Naamini tumeshasikia watoto wakijifu kupitia majina hayo ya wacheza filamu.
Hii ina maana kwamba, filamu za waigizaji hao zimesaidia kwa kiwango kikubwa kuwajenga watoto katika ujasiri unaoweza kuwa mfano mmoja tu wenye faida na motisha unaopatika kwenye filamu na hivyo kutia nguvu mada hii kwamba, tunaweza kuwahamasisha vijana wanaochipukia kuwa akina Rais Julius Nyerere, Kwame Nkrumah, Nelson Mandela kwa kuwapatia filamu za viongozi hao na kuzitazama.
Kama hilo halitoshi wanasaikolojia wanaamini kwamba, mtu anaweza kujitibu mwenyewe tatizo la msongo wa mawazo kwa kuangalia filamu zenye ujumbe unaohusiana na tatizo lake na hivyo kujiongezea moyo wa ushindi kupitia waigizaji anaowataza kwenye sinema.
Kwa mfano, mtu anaweza kuwa mgonjwa miaka sita na akawa katika hali ya kutaka tamaa lakini akiletewa filamu inayomuonyesha mtu mwenye ugonjwa kama wake akihangaika na hatimaye kupona hata yeye atafarijika na kuamini kuwa ipo siku atapona kama yule muigizaji na hivyo kupata imani ambayo itamsaidia kuishi.
Ninachotaka kueleza hapa ni kwamba , filamu hutengeza ndoto za maisha, huleta ubunifu na kuamsha hamasa ya kufikia malengo yetu, hivyo si busara kuipuuza tasnia ya uigizaji kwa mtazamo kuwa inawapotezea watu muda wa kutafuta mafanikio.
Jambo muhimu la kuzingatia kama nilivyodokeza hapo mwanzo ni kuwa makini na uchaguzi wa filamu tunazotaka kuziangalia. Maana hakuna ubishi kwenye elimu hii kwamba mtoto akizoezwa kuangalia filamu za kikatili atabadilika na kuiga tabia ya ugomvi, vivyo hivyo wanaopendelea sinema za ngono zitawashawishi kufanya kitendo hicho lakini sinema za kuelemisha ni msaada mkubwa wa kukuza ufahamu wa watu.
Naamini, wazazi wengi wakitumia filamu zinazoonyesha mateso wanayopata watoto wa kike baada ya kupewa mimba wakiwa shuleni na baadaye kutengwa na familia zao wanaweza kufikisha ujumbe wenye nguvu kwa watoto wao wa kike zaidi ya wao kutumia ukali na vitisho.
Ukweli ni kwamba, filamu zina uwezo mkubwa wa kutengeneza hisia kama nilivyosema kuliko maneno ya moja kwa moja, ndiyo maana upo utofauti mkubwa kati ya ujumbe unaotumwa kwa njia ya wimbo na ule unaoweza kutolewa kwa njia ya sinema.
Kama hilo halitoshi, kusahau maneno ni rahisi zaidi kuliko sinema hivyo kutumia njia ya filamu kufundishia kunatajwa kuwa ni njia bora zaidi ya kutolea maelekezo hasa kwa watoto ambao kusahau ni jambo jepesi kwao.
Saturday, March 17, 2012
Utafiti:Utazamaji filamu ni tiba ya matatizo
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment