“Nashanga  mama mdogo ananichukia bure, tena hakuna kosa nililomfanyia lakini  hanipendi tu” Je, wewe nawe umekuwa miongoni mwa watu wanaodhani  unachukiwa bure?
Achana na hulka hiyo, hebu tambua ubaya wako kwa  kuangalia vidokezo vifuatavyo, ambavyo naamini ukivisoma kwa umakini  utagundua ni wapi unakosea hadi kufikia hatua ya kuchukiwa katika jamii.
Je,  inapotokea umesababisha wenzako wajisikie vibaya huwa unajisikiaje  moyoni mwako? Mfano ulikuwa katika mazungumzo ya kawaida na rafiki yako,  lakini kwa sababu za kibinadamu akapokea mazungumzo yako vibaya na  kufadhaika. Wewe unapotambua kuwa umemuondolea mwenzako furaha huwa  unajisikiaje moyoni? Kama huumizwi na tukio hilo tambua kuwa wewe ni mtu  mbaya.
Jiulize, katika maisha yako ni mara ngapi umewafanya  wengine wafurahi kwa kuwatatulia matatizo yao, kuwasaidia wakati wa  shida na kuwavusha kwenye hali ngumu za kimaisha? Au umekuwa mtu wa  kusubiri usaidiwe hata kwa vitu unavyoweza kuwasaidia wenzako?
Tangu  umeanza kazi umeshawahi kutoa sehemu ya mshahara/pato lako kuwasaidia  wazazi na ndugu zako au umekuwa mtu wa kutoa visingizio vya hali ngumu  ya maisha licha ya kuwa unafanya anasa mjini? Ikiwa hujawahi kuwasaidia  watu kupata furaha, fahamu kuwa unaishi na ubaya kwenye jamii,  jiandae  kuchukiwa.
Je, unaposikia wenzako wana shida huwa  unazichukuliaje?, je ni sehemu ya tatizo lako au hujiweka pembeni na  kuwaachia binadamu wenzako wamalize matatizo yao? Ukiwa hivyo hicho ni  kipimo kikubwa cha ubaya wako kwenye jamii unayoishi.
Umekuwa  ukitumiaje uwezo wako  wa mali au hata nguvu za mwili mbele ya wenzako?  Je, ni kwa kuonea na kuwakandamiza watu  uliowazidi? Ikiwa una tabia  hiyo anza kujihesabu kuanzia leo kwamba wewe ni mtu mbaya mbele ya  jamii.
Angalia mazungumzo yako, je yamekuwa ni ya kuwatia moyo  watu, kuwafariji na kuwaelimisha au umekuwa mtu wa kutoa matamshi ya  kudhalilisha, kuudhi na kuwavunjia heshima wenzako? Kama ulimi wako  unatoa maneno yenye ‘sumu’ usitegemee kupendwa.
Je, umekuwa mtu  wa haki, mwenye kuwatanguliza wenzako? Unaweza kutoa unachokitegemea ili  kumsaidia binadamu mwenzio? Ukiwa huwezi kufanya hivyo na umekuwa mtu  wa kukumbatia mali zako ujue wewe ni mbaya.
Toka ndani ya moyo wako  unafurahia jamii kuwa na umoja au umekuwa mtu unayechochea migawanyiko  baina ya watu wanaopendana? Endapo una tabia kama hiyo fahamu kuwa  matendo yako ni mabaya.
Ni mara ngapi umezuia hasira zako kwa  lengo la kuepusha migogoro? Unaweza kuvumilia kuonewa au umekuwa mtu wa  kulipa kisasi kwa kudhamiria kufanya mambo mabaya kwa makusudi licha ya  moyo wako kukuonya mara nyingi usifanye hivyo? Kama una tabia hiyo  tambua kuwa huo ndiyo ubaya wako kwenye jamii.
Baada ya kupitia  dokezo hizo chache, naamini msomaji wangu utakuwa umejifunza kitu na  kuanzia leo utahakikisha kuwa unafanya mambo ambayo yanaifurahisha jamii  na hivyo kuepukana kabisa na ubaya ambao una madhara makuwa kwenye  maisha yako.
Saturday, March 17, 2012
Je ni Kweli Unachukiwa Bure?
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment