Saturday, March 17, 2012

Kwa Nini Babu Zetu Hawakufa kwa Ugonjwa wa Saratani

Ni ukweli ulio wazi kuwa magonjwa ya saratani yameibuka miaka michache tu iliyopita na yameshika kasi katika miaka ya hivi karibuni.

Hapo zamani, enzi za mababu zetu zaidi ya miaka 1,000 iliyopita, kulikuwa hakuna magonjwa ya saratani au kansa kama inavyojulikana na wengi.

Ni ukweli ulio dhahiri kuwa vyakula tunavyokula kila siku ndiyo chanzo kikubwa cha magonjwa ya saratani na magonjwa mengine sugu, kama kisukari, shinikizo la damu na magonjwa ya moyo.

Vyakula vya asili havipewi nafasi tena na badala yake kila kitu tunachokula ni ‘refined’ (kimesafishwa) na tunadhani kwa kula vyakula ‘vilivyosafishwa’ ndiyo tunakula vyakula bora.

Mababu zetu hawakuwahi kufa kutokana na magonjwa ya saratani kwa sababu walikuwa wakila vyakula vya asili ‘visivyosafishwa’ vilivyopatikana porini, kama vile matunda, mboga za majani, vyakula vya baharini, wakiwemo samaki, nyama ya porini, wakiwemo ndege kama mbuni na vingine vingi vizuri.

Mlo wa aina hiyo umethibitika kisayansi kuwa ndiyo uliowafanya mababu zetu kuishi kwa miaka mingi na ndiyo hasa unaofaa kuliwa na binadamu wa sasa ikiwa kweli tunapiga vita adui maradhi.

Kwa bahati mbaya sana, milo mingi ya sasa imetawaliwa na sukari kwa wingi na iliyoondolewa virutubisho.

Tukila mikate, tunakula ambayo ngano yake ilishaondolewa viini lishe vyote, tukinywa maziwa tunakunywa yaliyopitia kwenye mitambo na kuondolewa lishe yote, kila kitu tunachokula ni hatarishi, tunaishi kwa kudra ya Mungu pekee.

Kama unahitaji kujiepusha na maradhi sugu, huna budi kujiepusha na ulaji wa sukari na vyakula vinavyotengenezwa kwa sukari nyingi pamoja na kujiepusha na ulaji wa nafaka zilizokobolewa pamoja na vyakula vyake.

Ulaji wako wa sukari hautakiwa kuzidi gramu 25 tu kwa siku.

Ukiweza kuzingatia hayo, kamwe huwezi kusumbuliwa na maradhi kiasi cha kuona ni sehemu ya maisha yako na kwamba kila mtu ni lazima augue.

Pendelea kula vyakula vibichi zaidi kuliko vya kupika, mfano pendelea kula nyanya mbichi kuliko iliyopikwa au karoti mbichi kuliko ya kupika, n.k.

MAZOEZI


Utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na jarida la ‘Lancet’, umeonesha kuwa mazoezi ni sehemu muhimu sana ya kuimarisha afya ya mtu na kumuepusha na maradhi.

Imeelezwa kuwa mazoezi ya dakika 15 huongeza umri wa kuishi kwa miaka 3, hata kama uko katika hatari ya kupatwa na ugonjwa wa moyo.

Halikadhalika, wale wasiopenda kufanya mazoezi, wako katika hatari ya kupatwa na maradhi kwa asilimia 17 zaidi ya wanaofanya mazoezi.

Maradhi ya kisukari kwa mfano, yanaelezwa kusababishwa kwa kiasi kikubwa na ukosefu wa mazoezi licha ya ulaji wa vyakula vingine vinavyochangia ugonjwa huo.

Hivyo, kila mtu anayejali maisha na afya yake anatakiwa kujiwekea utaratibu wa kufanya mazoezi ya angalau dakika 15 kwa siku kwa njia yoyote anayoweza ili kuujenga na kuupa kinga mwili wake dhidi ya maradhi.

Mazoezi yanachukua asilimia 20 na mlo sahihi unachukua asilimia 80 ya afya yako.

Related Posts by Categories



No comments:

Post a Comment