Ni watu wachache wanaofahamu umuhimu wa kuwa na rafiki katika maisha yao. Wengi kati yao wanajikuta katika makundi ya watu bila kujua faida ya kuwa na ushirikiano na wengine.
Uelewa mdogo wa wazazi/walezi umewafikisha katika hatua ya kuwazuia watoto wao kutembelewa na marafiki zao nyumbani na hivyo kuamua kuwafungia ndani ya geti kila wanapotoka shule kwa hofu kuwa marafiki watawaharibu tabia watoto wao.
Inawezeakana wazazi wakawa sahihi endapo tu marafiki wanaoambatana na watoto wao ni wabaya, lakini mtoto kuwa na rafiki mwenye akili darasani, adabu na ufahamu mkubwa ni jambo muhimu ambalo linafaida nyingi katika kusaidia malezi yake.
Neno rafiki huwezi kulitofautisha na Upendo, kwa kuwa tafsiri inayopatikana katika Kamusi ya Kiswahili Sanifu inabainisha ni 'Kupendana na kuaminiana na mwingine'. Hivyo basi kumzuia mtoto asipendane na kuaminiana na mwenzake ni kumdumaza akili.
Uchunguzi unaonesha kuwa baadhi ya wazazi nao si rafiki wema kwa watoto wao kwa maana ile ya kamusi ya kupendana na kuaminiana. Lakini wengi wao wanaishi kwa desturi iliyotokana na uzazi tu. Upo ushahidi mwingi juu ya wazazi ambao wanaishi na watoto wao kama marafiki wabaya wakiwakosea adabu na kuwafundisha mambo ya kihuni.
Kama hilo halitoshi watoto hasa wanaosoma shule, mara nyingi wamekosa msaada wa kirafiki kutoka kwa wazazi wao kutokana na watu wanaoishi nao kuwa katika masumbufu ya dunia kupita kiasi au wakati mwingine ukali uliopindukia, jambao ambalo huwafanya watoto waishi ndani ya familia kama watumwa na hivyo kuwa na kiu ya kufarijiwa na watu wengine ambao ndiyo marafiki tunaozungumzia habari zao.
Kwa maana hiyo ili mwanafunzi/mwanadamu wa kawaida afikie kilele cha furaha, lazima awe na marafiki wa kupendana nao (simaanishi wapenzi wa kingono). Hawa ndiyo watakaomfariji atakapokuwa na msongo wa mawazo, watakaomfanya acheke, watakaomshauri, watakaomsukuma awe mtu mwema.
Ni wazi kwamba mtoto hawezi kufahamu mambo ya ulimwengu kwa kufungiwa ndani na mara nyingine kufanya hivyo ni kujaribu kuzuia jambo ambalo halizuiliki katika ulimwengu huu wa utandawazi.
Thursday, March 15, 2012
Umuhimu wa kuwa na marafiki
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment